Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amewataka wanasiasa nchini kujifunza siasa za kuvumiliana vinginevyo Tanzania itakuwa taifa la hovyo.
Nape ameeleza kuwa ili taifa liende mbele wanasiasa wanapaswa kujifunza kuvumiliana hata wanaposikia maneno wasiyoyapenda.
Mwanasiasa huyo aliyasema hayo juzi katika ibada ya kuaga mwili wa Victor Kimesera, mmoja wa waasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliyefariki dunia Machi 24 kutokana na ugonjwa wa saratani ya tumbo.
“Kimesera alikuwa mwanasiasa wa aina yake na alivumilia mengi. Hivyo, tunapaswa kujifunza siasa ya kuvumiliana. Hata kwa maneno tusiyoyapenda. Maana hii Tanzania bila kuvumiliana itakuwa nchi ya hovyo sana,” alisema Nape.
Aliongeza kuwa alikutana na Kimesera jijini Dar es Salaam walipokuwa wakicheza gofu katika viwanja vya Gymkhana na kwamba walikuwa wakitaniana na wakati wote marehemu alimsisitiza, “sisi ni wamoja inabidi tuishi kwa kuvumiliana.”
Nape alieleza kuwa marehemu alikuwa mwanasiasa mfano wa kuigwa aliyevumilia mengi katika harakati za kisiasa. Alieleza kuwa alikuwa rafiki yake waliyenunuliana vinywaji wakiwa kwenye viwanja vya gofu.
Tukio la kuaga mwili wa kimesera lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na Serikali. Baadhi ya waliohudhuria ni pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye; mkuu wa mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita.